top of page

ENURESIS (KUJIKOJOLEA) KWA WATOTO

“ Mwanangu wa kiume anatimiza umri wa miaka 6 hivi karibuni, na amekuwa akishindwa kuacha kujikojolea usiku alalapo, siku zote amekuwa akijikojolea sana kitandani kuliko kaka zake wawili ambao hawajawahi kuwa hivo. Mtoto mdogo wa dada yangu ambae ana umri wa miaka 13 hivi sasa, ana tatizo hili pia. Hali hii hunipa sana wasiwasi, endapo mwanangu atashindwa kuacha tabia hii kabla hajafika umri ambao ataanza kwenda kulala nyumbani kwa marafiki zake au yeye kukaribisha rafiki zake kuja kulala kwetu. Kuna muda hupita zaidi ya wiki 2 bila kujikojolea kitandani, nami huanza kuhisi pengine tatizo limeisha, lakini kwa bahati mbaya hali hii hujirudia”

Hayo ni maneno ya mama wa watoto watatu, juu ya tatizo la muda mrefu, la mwanae mdogo.


 

Enuresis ni hali ya kibinadamu ya kushindwa kuzuia kutoa mkojo katika kibofu katika sehemu na muda usio sahihi. Hali hii inategemea umri na muda inapotokea.


Kwa watoto chini ya miaka mitatu, ni kawaida kabisa kushindwa kujizuia kukojoa. Kujikojolea kitandani inakua Enuresis pale ambapo inatokea kwa mtoto zaidi ya umri wa miaka 4 (ikotokea mchana) na zaidi ya miaka 6 (ikitokea usiku) au mtoto kupoteza kujizuia baada ya miezi mitatu ya ukavu.


Muongozo wetu wa matibabu nchini wa mwaka 2021, unarejea Enuresis kuwa ni hali ya kujikojolea mara kwa mara kwenye kitanda au nguo (iwe kwa hiari au kwa makusudi)

na

Yenye kujitokeza kwa zaidi ya mara mbili kwa wiki kwa angalau miezi mitatu mfululizo

au

Uwepo wa dhiki kubwa ya kliniki au uharibifu katika jamii, kitaaluma, kikazi au maeneo mengine muhimu ya kiutendaji, umri wa mpangilio ni angalau miaka 5 (au kiwango sawa cha ukuaji).


Enuresis kwa kawaida hujitokeza wakati wa usingizi, kwa watoto wenye umri wa miaka 5 au zaidi, kushindwa kutunza mkojo katika kibofu.





Je, kukojoa kitandani ni kawaida kwa watoto?


Asilimia 25 ya watoto hulowesha vitanda vyao hadi umri wa miaka 3. Kwa umri wa miaka 6 hali hii hupungua hadi 15% tu, wakiwa na umri wa miaka 10 ni 5%.


Asilimia 0.5 hadi 1 ya watoto huendelea kulowesha vitanda vyao mara kwa mara hadi wanapokuwa na umri wa miaka 12-19 mpaka hali hii inapo jisuluhisha yenyewe.


Kukojoa kitandani kuna sehemu kubwa ya uhusiano kifamilia. Ikiwa wewe (kama mzazi) umelowesha kitanda ukiwa mtoto, mtoto wako anaweza kuendelea kulowesha kitanda pia. Hii mara nyingi ni sehemu ya kawaida ya maendeleo.


Nini hutokea mpaka kusababisha hali hii?


Kuta za kibofu cha mkojo ambacho ndio hifadhi ya muda mfupi ya mkojo, hujikaza na kulazimisha kuutoa mkojo, kutokana na sababu za kifiziolojia, kisaokolojia au vinasaba vya kifamilia.


Je, ni zipi sababu kubwa zinazo sababisha Enuresis kwa watoto?


Matatizo ya kibofu; kama vile, shughuli nyingi za misuli ya detrusor (detrusor muscle hyperactivity), ujazo mdogo wa vibofu kwa baadhi ya watoto na matatizo ya neva za kibofu ni moja ya sababu kubwa.


Vinasaba vya kifamilia: chunguzi zinaonesha uwiano wa jumla wa uwezekano wa kuwa na enuresis ya usiku ni mara 10.1 zaidi ikiwa baba au mama pia alikuwa na historia ya enuresis ya usiku.


Matatizo ya kisaikolojia; Kitabibu tatizo hili limejumuishwa kwenye magonjwa ya afya ya akili huku likihusishwa na ubora wa usingizi na msisimko wa mtoto. Ubora duni wa usingizi, harakati za mara kwa mara wakati wa kulala, na ukosefu wa usingizi wa kutosha ni mambo yanayohusiana na enuresis kwa mtoto. Tatizo hili pia hujakuathiri saikolojia ya watoto ambao mpaka kufikia balehe yao bado wanapatwa na hali hii na kupata sonona ambayo huongeza ukubwa wa tatizo.


Matatizo mengine ambatani ya kiafya; kama vile; kuvimbiwa, tatizo la kisaikolojia la ADHD, maambukizi ya njia ya mkojo, na apnea ya usingizi.



Je, nifanye nini kumsaidia mwanangu ambae bado anajikojolea kitandani?

  1. Punguza kiwango cha maji anachokunywa kabla ya kulala (angalau masaa 2)

  2. Ondoa vichochezi vyovyote vya chakula au kinywaji ambavyo huenda umeona vinaongeza uwezekano wa kukojoa kitandani.

  3. Mhakikishie mtoto kwamba si jambo la kuona aibu na kwamba hatimaye atashinda tatizo hilo.

  4. Tumia mfumo wa kengele kumwamsha mtoto wako au umwombe daktari akuandikie kifaa cha kengele kinachotumiwa kumwamsha mtoto. Njia hii imeonekana kusaidia zaidi ya 75% ya watoto wanaoitumia kwa zaidi ya miezi mitatu.

  5. Hakikisha familia, marafiki, wanashule na ndugu hawamchokozi au kumsema vibaya mtoto wako kuhusu suala hilo na pia apewe zawadi pale anapo onesha juhudi kuwa mkavu alalapo.

  6. Chunguza na ushughulikie tatizo lolote la kijamii la kifamilia au kielimu ambalo linaweza kuwa linampa msongo wa mawazo mtoto.

  7. Pokea usaidizi kutoka kwa madaktari na kupitia kliniki maalumu za watoto iliyopo karibu, ili mtoto aweze pitia chunguzi sahihi kubainishi chanzo cha tatizo.





Je, Tatizo hili linatibika?


NDIO, tatizo hili huweza kutibika kupitia njia za madawa tiba na pia mabadiliko ya tabia za kimaisha, baada ya daktari kubaini chanzo cha tatizo, ukubwa wa tatizo na hivyo kuweza kujua namna ya kulitatua tatizo.


Kukojoa kitandani ni hali inayo athiri kijamii na inaweza kudhuru zaidi kisaikolojia, haswa ikiwa itaendelea baada ya balehe ya mtoto na kwa ujumla ni hali inayoweza kutibika ikiwa haitajisuluhisha yenyewe mapema.


Hitimisho


Kutokana tatizo hili kuwa na uhusiano mkubwa sana na athari za kisaikolojia yanayoathiri ukuaji wa mtoto, tumejikita katika kutoa elimu itakayosaidia malezi na afya bora za watoto na watu wote kiujumla. Piga au tuma Whatsapp 0763 1000 93 kama unatafuta huduma au kwa swali lolote.

445 views0 comments
bottom of page