Kwanini Afya Ya Msingi Ndio Suluhisho La Tiba na Afya Bora Tanzania
Afya ya msingi (primary care) na kinga ni kiini cha mfumo wa afya Duniani. Upatikanaji wa huduma hii kwa urahisi ni chachu ya mafanikio ya sekta ya afya kwa jamii.
Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia mabadiliko makubwa ya sekta ya afya kwenye madaraja ya juu ya utoaji huduma, kama huduma za madaktari wabobezi, upasuaji, tiba za wagonjwa mahututi na mfumo mzima wa utoaji wa huduma izi. Kwa daraja la kwanza yaani afya ya msingi na kinga, maendeleo yameonekana zaidi kwenye muindombinu.

Tatizo la upatikanaji wa Afya liko wapi?
Wakati sekta afya zikiwa na mwelekeo huu, jamii pia imefuata. Wagonjwa wanatafuta madaktari bingwa au vituo vya utoaji huduma vyenye hadhi ya juu iwezekanavyo kupata huduma hata za ngazi ya msingi. Wengi wetu hatuna mazoea ya kuunda uhusiano wa kudumu na mtoa huduma mmoja. Changamoto za Upatikanaji wa huduma za afya kulingana na wataalamu na miundombinu iliyopo sio swala la uhaba kama ilivyo kua zamani. Jamii yetu imeendelea sana na tumefika mahali ambapo huduma zote za muhimu za afya zipo. Huduma za afya zinapaswa kuakisi maendeleo haya kwa mtoa huduma na mteja wake.
Namna ya kutumia wataalamu na miundombinu hii ndio kitendawili.
Mfano; Unapo kwenda kliniki, ili mtoa huduma afanye maamuzi sahihi ya tatizo lako la kiafya na mpango wa matibabu anahitaji kwa ujumla mambo mawili. Moja; Taarifa na Ushahidi wa sayansi juu ya tatizo lako la kiafya na pili; Ufahamu juu ya hali halisi ya Maisha yako kama mteja/mgonjwa. Jambo la pili linahitaji uhusiano wa karibu kati ya daktari na mteja wake. Ikiwa ni vigumu kujenga uhusiano huo na kila daktari, kuwa na muendelezo wa kupata huduma kwa daktari mmoja anae ratibu mahitaji yako ya kiafya ni rahisi.
Dhana ya kuwa na daktari mmoja kwa familia
Fikiri kama, kila unapo hitaji huduma za kiafya unasikilizwa na daktari mmoja. Labda ni maumivu ya kichwa yanayotokana na Malaria au ni tatizo la Sukari linalo sumbua wanafamilia. Unapo hitaji rufaa kwenda hosipitali au kwa daktari bingwa anakupa dira kulingana na ufahamu wake juu ya hali yako. Hudhani kama utapata huduma timilifu Zaidi na yakuridhisha?
Tafiti Zinasemaje?
Tafiti zinaonyesha muendelezo wa kupata huduma kwa daktari mmoja kila unapo hitaji huduma za afya (continuity of care) kunaongeza tija kwenye tiba utakayopatiwa na kuokoa gharama kwako na kwa mfumo wa afya kiujumla. Utafiti uliofanyika nchini Norway ulionyesha; muendelezo wa kupata huduma kwa daktari mmoja kuna husiana na kupunguza vifo, kulazwa wodini na uhitaji huduma za dharura. Utafiti huu ulionyesha Zaidi kwamba; muendelezo huu ukifika au kuzidi miaka 15, unapunguza changamoto hizi za kiafya kwa 25-30%.
Wakati wa ugonjwa ni akili ya kawaida kwa wengi wetu kutafuta daktari mahiri . Lakini, je wajua? Kama daktari huyo hajui changamoto za Maisha yako, mapenzi na matakwa yako, mtazamo wako juu ya hali ya uzima na ugonjwa,nk., hana taarifa za kutosha kuweza kutumia umahiri wake kikamilifu kukusaidia ?
Kuna dhana kwamba daktari binafsi au daktari wa familia ni ufahari. Na Thomas Carlyle aliwahi kusema,
“Mwenye afya ana tumaini, na mwenye tumaini ana kilakitu”
Ni ajabu jinsi ambavyo gari yako ina fundi au garage unayo iamini kwa ukarabati au matengenezo, lakini mwili wako unapo hitaji huduma hizi unatafuta sehemu au mtu yoyote atakae patikana kiurahisi.
Mtazamo
Miezi ya hivi karibuni tumeuliza watu wengi wa kipato, Imani na mazingira tofauti ya kimaisha juu ya namna wanavyo tafuta huduma za afya. Ingawa kuna tofauti nyingi kati yao, wengi wao wana mpango endelevu wa kujali uzima wa mali zao lakini hali ni tofauti juu ya uzima wa afya zao.
Wataalamu wana bobea kutibu magonjwa kwa uthabiti, na mfumo mzima wa afya una unajizatiti kukujali kwa ukamilifu zaidi ukiumwa. Hivyo mimi nadhani, kuchukua hatua za kujikinga na kuwa na mtu wa kukupa muongozo wa kuweza kutumia umahiri wa wataalamu na mfumo huu wa afya ndio jibu la kitendawili. Na ni wakati gani bora kuchukua hatua zaidi ya sasa?
Wakati nchi za magharibi zikijadili juu ya uganga kiusahihi (precision medicine), sisi bado tupo hapa tulipo. Lakini haipaswi kua ivyo, Dunia ni Kijiji. Maendeleo ya kaya moja ni maendeleo ya Kijiji. Kwenye sekta ya afya hii bado ni dhana tu, hasa kwa watu tulio chini ya jangwa la Sahara.Kuwa na muendelezo wa kupata huduma kwa mtoa huduma mmoja ni hatua ya kwanza kwenye juhudi za hudhihirisha dhana hii kua halisi.